Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Angelah Kairuki amesema wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuboresha sekta ya Elimu Nchini, ameyasema hayo leo Agosti 14, 2023 wakati wa kikao maalum na wadau mbalimbali wa elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa Anatoglo Mnazimmoja- Wilaya ya Ilala.
Akiongea wakati wa wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amesema Mkoa umetekeleza maagizo ya Mhe Rais ya kukaa na wadau wa maendeleo hususani wadau wa elimu kwa lengo la kuhamasishana kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu na mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji hapa nchini
RC Chalamila amesema Rais Mhe Dkt Samia ameendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya Elimu kuanzia elimu Awali, Msingi, Sekondari hadi vyuo vikuu, ambapo elimu ya Awali hadi kidato cha sita elimu inatolewa bila malipo na vyuo vikuu wanafunzi hupatiwa mikopo ya elimu ya juu.
Hata hivyo idadi kubwa ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka kutokana na maboresho yanayofanyika na Mhe Rais ambayo huamasisha wazazi wengi kupeleka watoto Shule na kuleta Changamoto ya kutokutosheleza kwa miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa, maabara, Maktaba, nyumba za walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, matundu ya vyoo na mabweni hivyo kikao hiki na wadau wa elimu kinalenga kutoa Suluhu ya Changamoto Katika Sekta ya elimu lazima tujiulize " Kama sio leo ni lini na kama Sio sisi ni nani" Alisema RC Chalamila
Kwa Upande wa Waziri wa OR-TAMISEMI amesema pamoja na mafanikio makubwa ambayo Serikali imeyapata katika sekta ya elimu bado kuna uhitaji mkubwa wa kuendelea kuboresha miundo mbinu ambapo takribani shilingi Trioni 17, 357,785,450,000.00 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya Awali, Msingi, Sekondari, shule za ufundi, elimu maalum, nyumba za walimu, na ukamilishaji wa miundombinu.
Hivyo Global Partnership for Education (GPE) wameendelea kusaidia Serikali ya Tanzania kupunguza Changamoto mbalimbali zilizoko katika sekta ya elimu nchini ambapo Tanzania imepata fursa ya kuomba ufadhili katika awamu ya tatu ambapo kigezo kikumbwa ni lazima wadau wazawa waonyeshe nia ya dhati ya kufadhili maboresho katika Sekta ya elimu kwa kujitoa kuchangia maboresho hayo.
Vilevile OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya elimu inaendelea na maandalizi ya hafla ya kuhamasisha wadau wa ndani Kufadhili maboresho ya sekta ya Elimu hafla ambayo inatarajiwa kufanyika Mkoa wa Dar es Salaam tarehe 31/08/2023 Mgeni rasmi anarajiwa kuwa Mhe Jakaya Mrisho Kikwete Rais Mstaafu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Anuani ya Posta: S.L.P. 5429
Simu ya mezani: +255 22 2203158
Simu ya mkononi: +255 22 2203156
Barua pepe: ras@dsm.go.tz
Haki Miliki © 2017 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,haki zote zimehifadhiwa