Hifadhi ya Mazingira
Manispaa ya Temeke imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na utalii. Temeke imezungukwa na ufukwe wa bahari wenye urefu wa km. 70. ukanda huu ni kivutio kikubwa cha utalii. Aidha, Manispaa ina machimbo ya Mchanga, Kifusi, Kokoto, Mawe na Chokaa .
Maeneo yanayotoa madini hayo na aina yake ni kama ifuatavyo:
Chamazi – Mchanga.
Mbande – Mchanga.
Kimbiji – Mchanga.
Toangoma - Mchanga
Mjimwema – Kokoto, Mawe, na Kifusi.
Kutokana na ukuaji wa kasi wa shughulli za ujenzi katika Manispaa ya Temeke na maeneo mengi ya Jiji la Dar Es salaam , mahitaji ya rasilimali hii yanaongezeka mwaka hadi mwaka hasa ukizingatia kwamba Manispaa ina rasilimali nyingi zenye ubora wa hali ya juu kulinganisha na Manispaa nyingine za Jiji la Dar Es salaam. Ili kuepuka wananchi kuchimba madini hayo kiholela katika maeneo yasiyostahili na kuleta madhara makubwa Kimazingira na Kiuchumi, imependekezwa kuwe na maeneo maalumu ya uchimbaji madini hayo ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato.
Baadhi ya maeneo yaliyofungwa ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato ni Kisarawe II, na Vijibweni kwa Manispaa ya Temeke.
Pia kufungwa kwa machimbo ya Kunduchi, Manispaa ya Kinondoni ambayo yalikuwa yanatoa madini ya kokoto na kifusi kwa kiasi kikubwa kwa jiji la Dar es Salaam, imepelekea kutafutwa eneo jipya la Madini ambalo imependekezwa machimbo hayo yahamie Mbutu na Mwongozo katika Manispaa ya Temeke. Tafiti zimefanyika kwamba maeneo hayo yatakidhi mahitaji ya kokoto na kifusi kwa jiji la Dar Es Salaam na uharibifu wa mazingira na upotevu wa mapato utakuwa rahisi kudhibitiwa. |