Katika maeneo ya pembezoni mwa Jiji, kilimo ni sehemu kuu ya kupata chakula na mapato. Mazao makuu ya chakula yanayolimwa ni mhogo, viazi vitamu, mpunga, mahindi, migomba na mikunde. Mazao ya biashara ni mikorosho, minazi, na matunda. Aidha, kutokana na uhaba wa ardhi Mkoa unasisitiza kilimo cha mboga matunda na viungo mazao yanayotumia eneo dogo la ardhi na kutoa mapato mengi kwa eka ambayo ni mananasi, machungwa na miembe, mboga na matunda mengineyo. Mazao haya yana soko la uhakika hapa Jijini.
Mahitaji ya chakula kwa mwaka ni tani 1,053,000. Mazao ya chakula yanayozalishwa hapa Mkoani huchangia 17% - 20% ya mahitaji ya chakula kwa mwaka. Aidha, asilimia 80% - 83% ya mahitaji ya chakula hutoka Mikoa mingine na nje ya nchi.
Hali ya kilimo cha pembezoni mwa Jiji bado ni duni ambapo kiwango cha kutumia zana za kilimo ni kidogo na matumizi ya pembejeo za kilimo sio mzuri kutokana na uwezo mdogo wa wakulima. Hata hivyo, hali ya upatikanaji chakula hapa Jijini na vijijini haina tofauti kutokana na wakulima kuhifadhi mazao mashambani kwa mfano mihogo, viazi vitamu na mpunga. Mihogo na viazi vitamu hupandwa nyakati tofauti na kuhifadhiwa ardhini. |