JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA - OFISI YA WAZIRI MKUU - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA      
 
     
 
     
ELIMU
 
Elimu [ Nyumbani ] au
 
 
Hali ya Maendeleo ya Elimu katika Mkoa
 

Idadi ya watu katika Mkoa wa Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa sababu ya shughuli za Viwanda na Biashara zinazofanyika. Mkoa una taasisi nyingi kuliko Mikoa mingine. Kwa ajili hii uwiano wa watoto nao ni mkubwa kuliko Mikoa mingine. Hali hii inasababisha idadi kubwa ya wanafunzi katika Mkoa wa Dar es Salaam.

 
 
 
Elimu ya Awali:

Mkoa wa Dar es Salaam unatekeleza agizo la Serikali la kutaka kila shule kuwa na darasa la Elimu ya Awali. Mkoa una jumla ya madarasa 425 ambayo yako kwenye shule mbali mbali za Serikali na hata hivyo, Sekta binafsi imeweza kuanzisha madarasa hayo pekee bila ya kuyaunganisha na Shule binafsi . Idadi hii ya madarasa bado hailingani na idadi ya shule za Msingi zilizopo 458. Hali hii iinasababishwa na ukosefu wa maeneo ya kujenga madarasa hayo, kwa kuwa shule nyingi ziko Mjini na maeneo ya Shule ni madogo. Wanafunzi wa Elimu ya awali wanahitaji eneo la kutosha kwa kuwa hujifunza kwa vitendo zaidi ambavyo huhitaji nafasi kubwa. Uongozi wa Mkoa unaendelea kuzishauri halmashauri kujenga majengo ya ghorofa ili kuongeza idadi ya madarasa ya Elimu ya awali na maeneo mengine yaachwe wazi kwa elimu ya vitendo.

 

 

Sekta binafsi ina jumla ya shule za awali 144 ambazo zinatoa Elimu ya awali kwa lugha ya Kingereza (English Medium). Katika Shule hizi elimu hutolewa kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali
 
 

Elimu ya Msingi

Kwa sasa Mkoa una shule za Msingi 338 za Serikali na 120 zisizo za serikali . Idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa darasa la kwanza imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka huu 2009 Mkoa umeandikisha jumla ya watoto 65,713 (Wavulana 31,805, Wasichana 33,908) wenye umri wa kuanza Shule. Lengo la awali lilikuwa kuandikisha watoto 67,159 (Wavulana 33,091 , Wasichana 34,068), . Uandikishaji huu umezingatia maeneo wanakoishi watoto ili kuwapunguzia matatizo ya usafiri.

 
Mdondoko
 
Sera ya Elimu na Mafunzo ya ufundi ya mwaka 1995 inaelekeza kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule waandikishwe shule, wahudhurie na wamalize elimu ya Msingi. Hata hivyo lengo hilo la serikali bado linapatwa na vikwazo kwani kuna tatizo la mdondoko wa wanafunzi. Kwa mfano mwaka 2008 jumla ya wanafunzi 1895 kati yao wavulana 1077 na wasichana 818 hawakumalizi elimu ya msingi kwa sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo, mimba na Ugonjwa.
 

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM).

 

Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ulianza kutekelezwa Mkoani kuanzia mwaka 2001.

 
 

Kutokana na mafanikio haya, Mkoa umeweza kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na pia kununua vitabu na vifaa mbali mbali vya kufundishia.

Aidha, maboresho haya yamewezasha kuongeza uwezo wa kuwapatia watoto nafasi za kusoma; kwa mfano mwaka 2006 Mkoa uliandikisha wanafunzi 60,411 ambao walianza darasa la kwanza mwaka 2007. Kiwango hiki cha uandikishaji kilikuwa ni sawa na asilimia 96.7 ya watoto 62,411 waliotarajiwa kuandikishwa.

 
Elimu ya Msingi kwa Walioikosa

 

Wapo watoto ambao kwa sababu mbalimbali hawakupata bahati ya kupata elimu ya msingi katika umri unaostahili. Kwa kuelewa kuwa elimu ni haki ya msingi na ya muhimu kwa kila mototo, serikali ilianzisha mpango wa elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA).

Mpango huu umegawanywa katika makundi mawili yaani kundi rika la kwanza kwa watoto walio kati ya miaka 10-13 na kundi rika la pili lenye vijana wa miaka 14-18. Vijana hao husoma kwa miaka 2-4 kisha wanafanya mtihani wa darasa la IV.Wanaofaulu hujiunga na elimu ya mfumo rasmi na baadhi yao ambao walidondoka njiani kisha kujiunga na MEMKWA huruhusiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wakifaulu huendelea na elimu ya sekondari.

 
 

 

 
 
Elimu ya Sekondari

Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya 1994 ulikuwa na Shule za Sekondari 7 tu, ambazo ni Kisutu, Jangwani, Kibasila, Forodhani, Pugu, Azania na Zanaki. Idadi hii iliuweka Mkoa huu katika nafasi ya mwisho Kitaifa katika kuwa na idadi ndogo ya Shule za Sekondari ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaofaulu. Hali hiyo ilisababishwa na Mkoa kutokujenga Shule za Sekondari kama Mikoa mingine.

 
 

 

Mkoa uliweka mikakati madhubuti ya kujenga shule za Sekondari. Hadi kufikia Aprili, 2009 Mkoa una jumla ya Shule za Sekondari 305 zikiwa Shule 125 za Serikali na 180 zisizo za Serikali.

 

Kati ya Shule 125 za Serikali, Shule 114 ni za Wananchi na Shule 14 ni mpya ambazo zimepata usajili tarehe 27/4/2009. Kati yake Shule 11 ni za Serikali Kuu na Shule 3 ni binafsi. .

 

Mgawanyo wa Shule za Wananchi za Kata ni kama ifuatavyo:-

 

Manispaa

Shule za Serikali Kuu

Idadi ya Shule za Wananchi

Ilala

09

39

Kinondoni

-

38

Temeke

02

37

Jumla

11

114

Aidha, Kata zisizo na Shule zinaendelea kutafuta maeneo ya kujenga Shule. Pia zipo Kata ambazo zinaendelea kukamilisha ujenzi wa Shule.

 
Elimu ya Watu Wazima:
 

Ilani ya Uchaguzi inaelekeza kuwa suala la kufuta ujinga miongoni mwa watu wazima lipewe umuhimu na msukumo mpya.

 
 
katika kutekeleza suala hili Sensa ya Watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu ilifanyika mwaka 2003. Watu walioandikishwa katika harakati za kufufua kisomo ni 32,191 katika kipindi cha mwaka 2005-7. Elimu ya Watu Wazima inaendelea kutolewa katika vituo 2,389.
Aidha madarasa 222 ya MEMKWA yenye idadi ya wanafunzi 13,707 yameanzishwa. .
 

MAFANIKIO YA MKOA:

 

Elimu ya Msingi:
Pamekuwa na mafanikio ya uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia kutoka Mpango wa MMEM ulipoanza mwaka 2001. Mafanikio haya ni pamoja na:-
•  Madarasa 2,520 yamejengwa katika Shule za Msingi.
•  Nyumba za Walimu 165 zimejengwa.
•  Matundu ya vyoo 1,452 yamejengwa.
•  Madawati 29,894 yametengenezwa.
•  Walimu 3,457 wa daraja la IIIA wameajiriwa. .

 
 
Elimu ya Sekondari:
  • Tumefanikiwa kujenga jumla ya shule 114 za wananchi.
  • Tumefanikiwa kupeleka wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kwa asilimia 76 sawa na wanafunzi 25,457 mwaka 2008
  • Tumefanikiwa kubuni Mpango wa Uchangiaji endelevu wa ujenzi wa sekondari
  • Tumefanikiwa kuhamasisha wananchi kuona umuhimu wa uchangiaji miradi ya Maendeleo.
 

CHANGAMOTO ZILIZOPO:

 
 

Pamoja na juhudi zinazoendelea za ujenzi wa majengo ya Shule, Mkoa unakabiliana na changamoto zifuatazo:-

•  Ukosefu wa maeneo ya ujenzi wa shule mpya katika Kata za mijini.
•  Gharama kubwa za kulipia fidia kwa ajili ya kupata maeneo ya kujenga shule
•  Mwamko bado mdogo kwa wananchi kuchangia maendeleo.
•  Mahitaji makubwa ya majengo na samani
•  Mfumuko wa bei katika vifaa vya ujenzi
•  Wanafunzi wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, mimba,utoro na vifo.
•  Kutokamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika baadhi ya shule kwa ajili ya kidato cha I-2008
•  Upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo katika baadhi ya shule na pia baadhi ya shule kukosa choo kabisa.
•  Kutokamilisha ujenzi wa majengo ya ghorofa.
•  Ukosefu wa nyumba za walimu, majengo ya utawala, maabara, Maktaba na Hosstel.
 
     
 
Elimu [ Nyumbani ] au
Rudi juu
 
     
Copyright © 2007 - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, TEL: 022 - 2203156/2203158, FAX: 022-2203158